Na
Albano Midelo
MTANDAO wa Kinga
Jamii Tanzania (TSPN) umempongeza mke wa
Rais wa awamu ya tano mama Janeth Magufuli kutokana na dhamira yake ya
kuwahudumia wazee wa Tanzania.
Pongezi hizo
zimetolewa na katibu mkuu wa TSPN Isikaka Msigwa wakati anazungumza na
waandishi wa habari mjini Songea.
Msigwa alisema
mtandao wa TSPN unatoa
pongezi za dhati kwa mama Janeth Magufuli kwa kuonesha moyo wa upendo mkubwa wa
kuwajali wazee wa Tanzania kivitendo ndani ya kipindi kifupi tangu serikali ya
awamu ya tano iingie madarakani.
“Ndugu
waandishi wa habari, Pongezi hizi za
kipekee kwa Mke wa Rais tunazitoa kwake kutokana na ukweli kuwa, ameonesha
moyo wa pekee wa upendo kwa wazee kwa
kutoa msaada mkubwa wa hali na mali katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwemo
Mkoa wa Dar Es Salaam na Shinyanga’’,alisisitiza.
Alibainisha
kuwa upendo huo umekuja wakati muafaka kwani ni wakati ambapo dunia na Tanzania
inapigania haki za wazee kwa nguvu zote ikiwemo haki ya kupata tiba, chakula,
malazi na huduma nyingine za msingi bila ubaguzi.
Takwimu
zinaonesha kuwa Wazee, ndiyo walezi wakubwa wa magonjwa ya muda mrefu, na zaidi
ya asilimia 50 ya watoto yatima hapa nchini hulelewa na wazee ambao kimsingi,
wao wenyewe wanahitaji kutunzwa kwa kuwa uwezo wao wa kuzalisha mali umepungua
na hata wale ambao bado wanajitahidi kuzalisha mali, hawapo kwenye kipaumbele
cha miradi mingi inayoendeshwa hapa nchini.
Utafiti
unaonesha kuwa vyombo vya kifedha vingi havitoi mikopo kwa wazee kwa kuhofia kuwa, mzee anaweza
kukopa lakini akashindwa kurejesha, na
kwamba wazee hawa hawana uwezo wa kumudu
masharti yanayowekwa na vyombo vya kifedha hata wakiwa tayari kuwakopesha.
Uchunguzi
pia umebaini kuwa wazee wengi nchini wana Rasilimali Ardhi ambazo hazina hati
miliki. Kutokana na changamoto zote hizo, wazee wengi wanatamani wasingendelea
kuishi baada ya kukata tamaa ya maisha.
“Kwa
wale wanaomwamini Mungu, watamuunga mkono Mama yetu Janeth Magufuli amechagua
fungu lililo jema kwani katika vitabu vya Mungu vinasisitiza kuwaheshimu wazee
na malipo kutokana na heshima hiyo, Mungu ameahidi kuanza kumlipa mtu huyo mema
kuanzia hapa hapa duniani’’,alisema Msigwa.
Ametoa
wito kwa Watanzania kwa ujumla, Taasisi, mashirika, makampuni na Serikali, kuanza
kuwapigania wazee kutokana na ukweli kuwa kila amb aye leo ni kijana hana
uwezo wa namna yoyote ile kuukwepa Uzee.
Hata
hivyo Msigwa alisema ni imani ya TSPN kuona Juhudi ambayo Mama Janeth Magufuli ameianza kuonesha mapema kabisa tangu Utawala
wa Serikali ya awamu ya tano kuwaunga mkono wazee,na kwamba hiyo ni nia ya
dhati ambayo Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kufanya katika kipindi cha miaka mitano kwa makundi tete wakiwemo wazee.
Alisema
Serikali ya awamu ya tano tayari imeweka
Wizara ambayo inashughulikia wazee, pia Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanzisha kauli mbiu
ya ‘’MZEE KWANZA’’ Alikuwa kama wewe utakuwa kama yeye’’
Ametoa
wito kwa serikali ya Tanzania kuongeza kasi katika kutunga na kupitisha Sheria ya
Wazee mwezi Septemba mwaka huu na kuanza kulipa Pensheni kwa Wazee wote kama
ilivyoahidi.
Alisema
Ili Tanzania iendelee kubarikiwa na mipango yake kwenda vizuri kama
inavyopangwa, Viongozi wengine Serikalini wamuunge mkono Mama Janneth Magufuli
kwa kuwaandalia Wazee mazingira mazuri kimaisha waishi kwa amani na furaha
katika kipindi ambacho wanaishi ili wasiondoke duniani huku wakiilaumu Serikali.
Katibu
mkuu huyo wa TSPN amewaasa watu binafsi, makampuni, jamii, taasisi nao waunge
mkono juhudi hizo za kuboresha maisha ya Wazee wa Tanzania kila mmoja alipo
bila kuisubiri Serikali.
Tanzania
Social Protection Network (TSPN), ni muungano wa Mashirika 34 yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa kisheria
kutoka mikoa 26 ya Tanzania bara na Visiwani, yanayojishughulisha na
kuwahudumia Wazee, Watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali na Watoto waishio
katika mazingira hatarishi, mtandao ambao ulioundwa rasmi mwaka 2010.
albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
No comments:
Post a Comment