Na Stephano Mango
Uwanja wa ndege wa Ruhuwiko uliopo manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma ni rasilimali adimu inayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea
hasa kutokana na uwanja huo kuwa ni
miongoni mwa viwanja bora Tanzania.
Uwanja wa ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja 13 bora
vya ndege Tanzania kati ya viwanja karibu 50 vilivyopo nchini.Uwanja huo ambao
ulijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 umewekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa
kutua ndege majira yote masika na kiangazi.
Utafiti umebaini kuwa uchumi wa manispaa ya Songea
umeongezeka ingawa sio kwa kiwango
kikubwa baada ya kuanza safari za anga
kutoka Songea hadi Dar es salaam ukilinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya
mwaka 2011 wakati mji wa Songea ukiwa hauna usafiri wa anga.
Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo anasema
Kabla ya kuanza safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Songea mwaka
2011,wafanyabiashara,Taasisi za kidini,wawekezaji na wadau wengine walikuwa
wanapata shida ya kusafiri kwa magari ambayo yanachukua zaidi ya saa 15 kutoka
Dar es salaam hadi Songea.
Midelo anasema safari za anga zimesaidia wadau mbalimbali
kutumia usafiri wa ndege kutoka na kwenda Dar es salaam hivyo kuwezesha kufanya kazi zao kwa muda mfupi
badala ya kupoteza saa kadhaa barabarani hivyo kuzorotesha uchumi wa manispaa
ya Songea na wa mtu mmoja mmoja.
“Licha ya kukuza uchumi,lakini usafiri wa anga katika
manispaa ya Songea umerahisisha huduma za matibabu,mgonjwa anapozidiwa na
kuhitaji rufaa kwa haraka anasafirishwa kwa njia ya anga kutoka Songea hadi Dar
es salaam,hivyo usafiri wa anga umesaidia kuokoa maisha ya wakazi wa Songea na
watanzania kwa ujumla wake’’alisema.
Ongezeko kubwa la wageni wanaosafiri kwa ndege katika mji wa
Songea wanapolala katika nyumba za wageni na kukodi taksi kutoka uwanja wa
ndege hadi mjini wanasaidia kuongeza pato katika Halmashauri ya manispaa ya
Songea.
Hata hivyo changamoto kubwa ambayo inasababisha wakazi wa Songea na wageni kutotumia usafiri wa
ndege ni nauli kubwa ambayo inatozwa na kampuni binafsi ya ndege ya Auric Air
ambayo ni kati ya shilingi 350,000 hadi 400,000 bei ambayo wengi wanashindwa
kumudu kulipa.
Utafiti unaonesha kuwa nauli za ndege zikishuka watanzania
wengi wanaweza kusafiri kwa ndege kutoka
Dar es salaam hadi Songea hivyo Songea itapata wageni wengi ambao watapata
huduma mbalimbali za usafiri,chakula,malazi na kutembelea vivutio vya utalii
hivyo kukuza pato la serikali na mwananchi mmoja mmoja.
![]() |
| Meneja uwanja wa ndege wa Songea Valentine Fasha |
Meneja wa uwanja wa ndege wa Songea Valentine Fasha amesema licha ya changamoto ya nauli
inayotozwa na kampuni binafsi ya ndege ya Auric air bado kuna idadi kubwa ya
abiria ambao wameamua kusafiri kwa ndege toka Songea hadi Dar es salaam.
“Abiria ambao wanatumia ndege kutoka Songea hadi Dar es
salaam wanaendelea kuongezeka kwa mfano kwa mwaka 2015 pekee abiria karibu 5000 walisafiri kwa ndege idadi ambayo
inaridhisha kwa kuwa kabla ya usafiri wa anga idadi ya wageni waliokuwa
wanafika Songea pia ilikuwa chini’’ ,alisisitiza.
Alisema ndege zilizokuwa zinatua kwenye uwanja huo kabla ya
mwaka 2011 zilikuwa zinakodiwa kwa gharama kubwa ambapo kuanzia Oktoba 17,2011
kwa mara ya kwanza ndege ya abiria ya Auric ilianza kutoa huduma kwenye uwanja
huo kuja Songea na kurudi Dar es salaam.
Hata hivyo amesema serikali itakaponunua ndege ya serikali
nauli ya ndege inaweza kupungua na kwamba lengo la mamlaka ya ndege Tanzania ni
kuhakikisha kuwa kila mtanzania aweze kusafiri kwa ndege kwa kuwa usafiri wa ndege ndiyo wa haraka,salama na uhakika zaidi.
Fasha amebainisha kuwa ndege ya Auric inatoa huduma za
usafiri siku tano kwa wiki ambazo ni Jumamatu, Jumanne, Jumatano, Alhamis na
Jumamosi, ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 13, inatumia saa 2.15 kutoka
Songea hadi Dar es salaam.
Hata hivyo amesema ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria
kuanzia 50 inatumia takriban saa moja tu kutoka Songea hadi Dar es salaam na
kwamba nauli kwa ndege kubwa pia inapungua ukilinganisha na ndege ndogo.
Kulingana na meneja wa uwanja huo,Mamlaka ya viwanja vya
ndege Tanzania ina mpango wa kupanua uwanja wa ndege wa Songea ambapo serikali
imefanya upembuzi yakinifu katika viwanja 11 Tanzania ukiwemo uwanja wa ndege
wa Songea ambavyo vinatakiwa kuboreshwa ili viweze kutoa huduma bora na za
kisasa na kusababisha ndege kushawishika kutoa huduma Songea.
Fasha amesisitiza kuwa uwanja wa ndege wa Songea unatarajiwa
kupanuliwa na kupewa vifaa vya kisasa ili uwe uwanja wa kisasa zaidi pia ni matarajio ya
serikali kuleta ndege ya serikali ambayo inaweza kuboresha huduma za usafiri wa
ndege katika safari ya Dar es salaam-Iringa hadi Songea.
“Route zote za ndege katika Tanzania zina huduma za ndege
isipokuwa hakuna route ya Dar es salaam,Iringa na Songea,Rais wetu Magufuli
amepania kulisimamia shirika la Ndege hivyo naamini atahakikisha route yetu
inafanikiwa,lengo ni kila mtanzania aweze kupanda ndege,aone dunia
inavyoonekana akiwa angani,aweze kusafiri kwa haraka kwa gharama
nafuu’’,alisisitiza.
Amesema shirika la ndege la Tanzania likifufuliwa na
kusimama utakuwa ni ukombozi kwa watanzania wote kwa kuwa sasa ndege zitaruka
na kutua katika kanda zote ikiwemo ya Dar es salaam,Iringa hadi Songea hivyo kufuta tabaka kwamba kila mmoja ataweza
kupanda ndege kutokana na gharama kuwa chini.
Katika bajeti ya mwaka 2016/2017,Waziri wa ujenzi,uchukuzi
na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema shirika la ndege Tanzania (ATCL)limetengewa
shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kununua ndege tatu mpya.
Hata hivyo Profesa Mbarawa alisema idadi ya ndege
zitakazonunuliwa na bei ya kila moja itajulikana baada uya uchambuzi
kukamilika.
Alisema mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania katika bajeti
ya mwaka 2016/2017 imetengewa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kutekeleza
miradi yake ikiwemo ukarabati wa viwanja vya ndege ,usimikaji wa taa,mitambo ya
kuongozea ndege na kuendeleza upanuzi wa viwanja vya ndege.
Mwisho




No comments:
Post a Comment