Na
Albano Midelo
UTAFITI uliofanywa
kwa miaka mitatu mfululizo katika nchi mbalimbali Duniani zinaonesha kuwa
Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa ukatili dhidi ya wazee.
| Bibi aliyeamua kujitengenezea jeneza lake |
Takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Haki za binadamu ambapo wazee wamekuwa wahanga
wa mauaji na manyanyaso yanayotokana na tuhuma za kishirikina ambapo wazee 2866
wameuawa kwa imani za kishirikina katika mikoa kumi katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita ikiwa ni wastani wa mauaji ya wazee 573 kila mwaka.
Matokeo ya tafiti
tatu zilizofanywa duniani kuanzia mwaka
2013 hadi 2015 na Shirika la Kimataifa la Help Age International (HAI) ambalo
limeendesha utafiti katika nchi zipatazo 96 duniani kuangalia hali ya usalama wa maisha ya
wazee duniani yanaonesha kuwa Tanzania
sio mahali salama pa kuishi wazee.
Utafiti ambao umefanywa na Help Age International katika
nchi 91 ambazo shirika hili linafanya kazi ambapo kwa mwaka 2013 nchi ya kwanza
kwa usalama wa wazee kuishi Duniani
ilikuwa Sweden na ya pili ni Norway zinaonesha wazi kuwa wazee wa
Tanzania wanaishi katika mazingira ambayo sio salama.
Katika utafiti huo Tanzania ilikuwa nchi ya 90 kati ya nchi 91 zilizofanyiwa utafiti huo
hali ambayo inathibitisha kuwa Tanzania sio mahali salama kuishi wazee.Katika
utafiti huo Nchi ya Afghanistan imetajwa kuwa ni nchi ya mwisho yaani ya 91 kwa
usalama wa wazee kuishi,Tanzania ikikamata nafasi ya pili kwa ukatili wa wazee
Duniani.
Hata hivyo utafiti huo wa kimataifa kwa Upande wa afya mwaka 2013 ulionesha kuwa nchi ya Tanzania
ilikuwa ya 73 kati ya nchi 91 takwimu
ambazo zinaonesha kuwa angalau kwa upande wa sekta ya afya kwa huduma za wazee
kuna maendeleo kidogo.
Kwa mwaka 2014 nchi ya kwanza kwa usalama wa wazee kuishi
ilikuwa Norway na ya pili ni Sweden wakati Tanzania
ilikuwa nchi ya 92 kati ya nchi 96
zilizofanyiwa utafiti huo.Matokeo ya utafiti huo yanaonesha wazi bado Tanzania
sio nchi salama kuishi wazee. Nchi ya Afghanistan katika mwaka 2014
imeendelea kuwa nchi ya mwisho (96) kwa
vitendo vya ukatili dhidi ya wazee Duniani.
Licha ya Tanzania kuwa
katika nafasi mbaya kwa usalama wa kuishi wazee Upande wa afya Tanzania katika
utafiti wa mwaka 2014 imeendelea kupanda na kushika nafasi ya 69 ukilinganisha nafasi ya 73 katika afya
mwaka 2013.
Katika utafiti wa mwaka 2015 nchi ya kwanza kwa usalama wa wazee
kuishi ilikuwa Switzerland na ya pili ni Norway wakati Tanzania ilikuwa nchi ya 91 kwa
usalama wa wazee kuishi kati ya nchi 96 zilizofanyiwa utafiti huo.
Nchi ya Afghanistan
bado imeendelea kushika mkia na
kuwa nchi ya 96 kwa usalama wa wazee
kuishi Duniani ambapo Tanzania katika utafiti huo kwa upande wa Afya imeendelea kuwa nchi ya 69 kati ya nchi
96 Ulimwenguni zilizofanyiwa utafiti huo.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika linalohudumia wazee la
PADI Isikaka Msigwa anasema kutokana na takwimu hizo Tanzania bado ni nchi
ambayo wazee hawatendewi haki ndiyo maana wazee katika baadhi ya mikoa wamekuwa
wanauawa kwa visingizio mbalimbali.
“Katika Sekta ya Afya licha ya Tanzania kupanda katika
huduma za afya kwa wazee , juhudi zaidi zinahitajika, lakini matokeo
chanya ya juhudi hiyo yameanza
kuonekana ni kutokna na nia dhati ya
serikali kutamka kuwa tiba bure kwa wazee wote licha ya changamoto zilizopo za
upungufu na wakati mwingine kukosa kabisa dawa’’,alisema Msigwa.
Hata hivyo Msigwa amesisitiza kuwa Tanzania Kimataifa imeonesha
kupiga hatua katika kutoa huduma bora
kwa wazee kwa kuzishinda nchi 18 kwa mwaka 2013, nchi 27 kwa mwaka 2014 na nchi
27 kwa mwaka 2015 kati ya nchi zaidi ya 90 zilizofanyiwa utafiti huu.
“Tanzania ili iweze kujiondoa katika nafasi karibu ya
mwisho ni lazima serikali itafutie ufumbuzi wa mauaji ya wazee pamoja na
kukabiliana na umaskini wa kipato ikiwa ni pamoja na kuanzisha Pensheni kwa
wazee wote kunaweza kuipandisha nchi kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira
rafiki kwa wazee kama ilivyo kwa nchi za barani Ulaya’’,alisisitiza.
Ameiasa jamii kurudisha upendo kwa wazee hatimaye kupungua au kumaliza kabisa kwa mauaji yanayotokana na kutowapenda
wazee kwa baadhi ya familia kutokana na
Umasikini wao na kwamba sera ya mzee kwanza inatakiwa kuenezwa kila kona ya Tanzania ili jamii yote iweze kubadilika kifikra na kimtazamo kuhusu wazee.
Kwa Mujibu wa sensa ya watu na makazi ya
2012, Wazee miaka 60 na kuendelea waliopo Tanzania ni asilimia 5.6 ya
watanzania wote ambao ni zaidi ya milioni 45 sawa na wazee zaidi ya 2.5 Kati yao
1,307,358 ni wana wake na 1,200,210 wanaume.
Idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka na kufikia
wazee milioni 8.3 sawa na asilimia 10 ya watanzania wote ifikapo mwaka 2050 na
kwamba mwaka 2050 duniani kunakadiriwa kuwa na wazee wengi zaidi kuliko wale
vijana wenye umri chini ya 14.
Katika bara la Afrika peke yake inakadiriwa kuwa na wazee zaidi ya milioni 38
kwa sasa na ifikapo mwaka 2050 kunatarajiwa kuwa na wazee zaidi ya milioni 212.
albano.midelo@gmail.com,simu
0784765917

No comments:
Post a Comment