Monday, May 23, 2016

Manispaa ya Songea yajipanga kuupokea Mwenge wa Uhuru



Na Julius Konala,Songea
Maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma yamepamba moto  kwa kuhakikisha miradi yote inayotarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa inakamilika.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Benson Mpesya akikagua stendi

Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo alisema Mwenge wa Uhuru katika manispaa hiyo unatarajiwa kuingia Juni 8,2016 ukitokea wilayani Namtumbo ambao utakimbizwa katika maeneo mbalimbali yenye miradi  na utakesha katika mtaa wa Kibulang’oma kata ya Lizaboni.


Kwa mujibu wa ratiba ya Mwenge wa Uhuru katika manispaa ya Songea,Juni 9,2016 yatafanyika makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Halmashauri ya manispaa ya Songea na Halmashauri ya mji wa Mbinga.

Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Songea ikiongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa wilaya hiyo Benson Mpesya pamoja na mkurugenzi wa manispaa ya Songea Jenifer Omolo inaendelea kukagua miradi yote ambayo inatarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa katika manispaa hiyo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa madawati katika shule ya msingi Luhira,kuweka jiwe la msingi mradi wa barabara ya lami ya FFU hadi Chemchem na uzinduzi wa nyumba ya mkurugenzi wa manispaa ya Songea.

Miradi mingine ni uzinduzi wa kituo cha mabasi cha mjini kati,uzinduzi wa  darasa la matokeo makubwa sasa(BRN) katika shule ya sekondari ya Chaburuma,mradi wa hifadhi ya mazingira Luhira na kukagua mradi wa kikundi cha ufugaji kata ya Mwengemshindo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ambayo inatarajiwa kuwekewa jiwe la msingi na kufanyiwa uzinduzi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru katika manispaa ya Songea,mkuu wa wilaya ya Songea Benson Mpesya amewaasa wakazi wa manispaa ya Songea kujitokeza kwa wingi siku hiyo hasa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru.

“Mwenge wa Uhuru wa sasa umelenga kuleta hamasa ya kuleta mabadiliko kwa kuhamasisha miradi mbalimbali ya maendeleo ili wakazi wa Songea na  watanzania kwa ujumla waweze kupata maendeleo ya kweli hivyo ni vema wakazi wa Songea kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo ambalo linatokea mara moja tu kwa mwaka’’,alisisitiza.

Mwisho

No comments:

Post a Comment