Saturday, May 14, 2016

Wilaya ya Nyasa kuanza kukimbia kiuchumi



Na Kwirinus Mapunda

WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma inatarajia kuanza kukimbia kiuchumi  baada ya serikali kutoa fedha za ujenzi wa Barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa takribani kilometa 65.
Mbunge wa jimbo la Nyasa Injinia Stella Manyanya

Mbunge wa jimbo la Nyasa ambaye pia ni Naibu waziri wa Elimu, Sayansi,teknolojia na ufundi injinia Stella Manyanya amesema bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 imeshatenga fedha kwa ajili ya upembuzi wa kina wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Lituhi hadi Kitai.

Hata hivyo amesema bajeti ya wizara ya ujenzi na mawasiliano ya mwaka wa fedha
wa 2016/2017 tayari zimetengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa kumi toka Kitai hadi Lituhi.


Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma  Laizeck Alinanuswe amesema serikali imepanga kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Chiwindi-Mbambabay hadi Lituhi ambapo mshauri elekezi anatarajia kuanza kazi ya upimaji kwa ajili ya matayarisho.
Kaimu meneja wa TANROAD mkoa wa Ruvuma Laizeki Alinanuswe

“Barabara kwa kiwango cha lami barabara ya Mpapa-Liparamba-Mipotopoto hadi Mitomoni,barua ilishaandikwa wizara ya ujenzi,uchukuzi na mawasiliano kwa ajili ya kuhakikisha barabara hiyo inajengwa’’,alisema.

Kwa mujibu wa kaimu meneja huyo wa TANROAD bajeti ya mwaka ujao wa fedha imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Likuyufusi hadi Mitomoni.

Katika hatua nyingine ambazo zinaweza kufungua mawasiliano wilayani Nyasa na kuifanya wilaya hiyo kuanza kukimbia kiuchumi ni ujenzi wa reli itakayoanzia Mtwara hadi Mbambabay wilayani Nyasa.

Mbunge wa jimbo la Nyasa injinia Stella Manyanya amesema tayari serikali imepitisha mpango wa ujenzi wa reli hiyo hivyo amewaasa wakazi wa jimbo hilo kujitayarisha ili waweze kukuza uchumi wao kuanza ngazi ya familia.

Kuhusu ujenzi wa daraja la mto Ruhuhu ambalo litaunganisha wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na wilaya ya Ludewa mkoani Njombe,injinia Manyanya amesema fedha ya kuanza ujenzi imetengwa katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja la mto Ruhuhu litaimarisha mawasiliano  baina ya wilaya hizo hali ambayo itasaidia kuimarisha uchumi wa wananchi hasa katika kilimo, usafirishaji na uvuvi.

Kwa miaka mingi wakazi wa Nyasa na Ludewa wamekuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuvuka mto Ruhuhu kwa mitumbwi kutokana na kivuko kutofanyakazi kwa kipindi kirefu hali iliyosababisha baadhi ya watu kufa maji katika mto Ruhuhu na wengine wakikamatwa na mamba wakati wanavuka mto huo.

Utafiti umebaini kuwa kivuko cha Ruhuhu kinafanya kazi kwa miezi mitatu tu kwa mwaka kinaanza mwezi Juni hadi Agosti,hali hiyo inatokana na serikali kushindwa kujenga gati bora kwa ajili ya kuweka nanga kivuko kinapotoka upande mmoja wa mto na kwenda upande mwingine.

Magari yanashindwa kuvushwa katika kivuko hicho hali ambayo inasababisha kuzunguka kutoka Lituhi, Songea hadi Njombe kisha Ludewa mjini safari ambayo inachukua siku nzima wakati kwa kutumia kivuko cha M.V Ruhuhu  ni mwendo wa saa moja hadi Ludewa mjini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa

Baadhi ya wakazi wa Lituhi na Ludewa walisema kivuko cha Ruhuhu ni kero ya muda mrefu ambayo hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete anaifahamu na aliahidi kuitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa inagharimu maisha ya watu kila mwaka pia inazorotesha maendeleo yao kiuchumi.

Julius Challe mwenyekiti wa kitongoji cha Lituhi anasema wakazi wa Lituhi wanapata matatizo makubwa kutokana na ukosefu wa huduma za kivuko cha Ruhuhu hawajui lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa ni tatizo la muda mrefu ambalo serikali imekuwa itoa ahadi zisizotekelezeka za kujenga daraja.

Wananchi wanaotegemea kivuko hicho kwa kiwango kikubwa ni kutoka vijiji vya Msungu,Ilela,Mbongo,Manda,Lupingu na Ngerenge wilayani Ludewa mkoani Njombe na vijiji vya Lituhi,  Nkaya, Mwelampya,Kihulu,Litumbakuhamba na Ngingama wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Serikali iliamua kununua kivuko cha Mv Ruhuhu kama suluhisho la muda wakati ikiendelea na mikakati ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja  ambalo litawahakikishia usafiri wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Akizungumzia kuhusu uimarishaji wa bandari na usafirishaji wa meli katika ziwa Nyasa kutoka bandari ya Itungi kupitia bandari za mwambao mwa ziwa Nyasa zikiwemo Manda,Ndumbi,Mkili,Liuli hadi Mbambabay injinia Manyanya alisema kazi ya ujenzi wa meli mpya katika bandari ya Itungi.

“Nilitembelea Itungi port Kyela  ili kufanya ukaguzi,nimeshuhudia Gati limekamilika na ujenzi wa meli mbili za mizigo tani 1000 kila moja na meli ya abiria unaendelea na bandari ya Ndumbi imeanza kujengwa’’,alisisitiza.

Kukamilika kwa miundombinu ya barabara katikakiwango cha lami na ujenzi wa daraja la Ruhuhu,reli pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa meli mpya kusaidia kuimarisha sekta ya usafirishaji katika wilaya ya Nyasa hali ambayo pia itasababisha wilaya ya Nyasa kuanza kukimbia kiuchumi.

kwirinusmapunda@yahoo.com

No comments:

Post a Comment