Saturday, July 2, 2016

Asilimia 92 ya nyumba za manispaa ya Songea ni bora

Nyumba nyingi za manispaa ya Songea ni bora

Na Julius Konala

Ukaguzi wa usafi na mazingira katika majengo na nyumba uliofanyika katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umebaini kuwa asilimia zaidi ya 92 ya nyumba katika manispaa hiyo  zilikuwa bora.


 Ofisa habari wa Manispaa ya Songea Albano Midelo alisema kuwa  manispaa hiyo ilifanya  ukaguzi wa usafi wa Mazingira   katika nyumba 2,674.
Kwa ajili ya kufuatilia usafi wa mazingira, ujenzi wa nyumba,vyoo bora, matumizi ya vyandarua, utunzaji wa maji katika Kaya pamoja
na visima vya maji majumbani.



“Lengo lilikuwa kukagua nyumba 2588 hata hivyo hadi kufikia Desemba 2015 nyumba 2565 zilikaguliwa sawa na asilimia 99.6, katika ukaguzi huo nyumba 2396 zilikuwa bora sawa na asilimia 92.90’’,alisema.



Katika kutekeleza agizo la Rais Dr.John  Magufuli la kufanya usafi wa mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi inafanya shughuli mbalimbali za usafi katika kata zote 21 na mitaa 95 inayounda manispaa hiyo.



Kwa mujibu wa Midelo kazi za usafi wa mazingira ambazo zimekuwa zinafanywa ni pamoja na  Kufagia, kukusanya takataka na kuzizoa kwenye maeneo ya makazi, biashara na Taasisi, kulima na kufyeka nyasi, kufukua mifereji ya maji ya mvua na kufukia mashimo na madimbwi.



Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanajengewa uwezo katika suala la utunzaji na usafi wa mazingira,Idara ya afya na mazingira inawaelimisha wananchi kuyaweka mazingira katika hali ya usafi kupitia vyombo vya habari pamoja na  kutumia gari lenye kipaza sauti.



Takwimu zinaonesha kuwa mwezi Desemba 2015 pekee katika manispaa ya Songea, tani zaidi ya 303 za taka ngumu zilikusanywa na kwamba tani zilizopelekwa dampo zilikuwa tani 194.



Amesema operesheni ya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi imekuwa inafanywa na wakazi wote katika manispaa hiyo  wakiwemo Majeshi,Watumishi wa Umma, Taasisi za Umma, Taasisi binafsi,Mashirika ya Umma, Asasi za kidini na asasi za kiraia.



Ili kukabiliana na wachafuzi wa mazingira,amesema,mashtaka na faini za papo kwa papo zimekuwa zinatolewa kutokana na faini za uvunjaji wa sheria mbalimbali za Afya na usafi wa mazingira,lengo likiwa ni kuuweka mji wa Songea katika hali ya usafi.



Pia kunafanyika Ukaguzi wa vyakula mbalimbali ili kutambua iwapo vina vifaa kwa matumizi ya binadamu na kwamba vyakula ambavyo havistahili vinaondolewa  ambapo tayari vyakula na vinywaji ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu vyenye thamani  ya zaidi shilingi milioni tano.



Hata hivyo amesema Elimu ya afya juu ya matumizi ya maji safi na salama inaendelea kutolewa kwa njia ya vyombo vya habari na mikutano ya hadhara ili kuepukana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.



MWISHO

No comments:

Post a Comment