Monday, July 4, 2016

St.Vincent shule iliyopewa cheti cha ubora wa elimu

Ni shule maalum ya bweni ya wenye ulemavu wa kusikia


St.Vinsenti shule ya msingi ya elimu maalum ya wenye ulemavu wa kusikia iliyowahi kupewa cheti cha ubora wa shule Tanzania mwaka 2000 kutoka wizara ya elimu  kutokana na kufaulisha karibu kila mwaka darasa zima.



Shule ya mtakatifu Vincenti inayomilikiwa na watawa wa kanisa katoliki imeanzishwa  katika kata ya Ruhuwiko manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

 Shule hiyo imejengwa katika viwanja ambavyo vilitumiwa na aliyekuwa kiongozi mkuu wa kanisa katoliki Duniani mwaka 1990  katika adhimisho la misa takatifu.Hayati  papa yohanne Paulo wa pili Septemba 1990 alifanya ziara ya kutembelea nchi kadhaa barani Afrika ikiwemo Tanzania
.



Miongoni mwa mikoa ambayo kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa kanisa katoliki Duniani aliweza kuitembelea na kufanya adhimisho la misa takatifu ni eneo la Ruhuwiko mjini Songea mkoa wa Ruvuma.



Kutokana na umuhimu wa ujio wa papa Yohanne Paulo wa pili kanisa katoliki jimbo kuu la Songea liliona umuhimu wa eneo hilo kuweka kumbukumbu ya ujio wa Papa ndiyo maana ikapendekezwa kujengwa shule ya bweni ya wenye ulemavu wa kusikia yaani viziwi inayoitwa St.Vincenti.



Mkuu wa shule hiyo Sr.Anna Mgaya anasema St.Vincent ni miongoni mwa shule ambazo zinatoa mchango mkubwa kwa wenye ulemavu hapa nchini inahudumia watoto wenye ulemavu katika kundi la viziwi.



Anabainisha kuwa shule hiyo inawahudumia wenye ulemavu viziwi kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya,Dar es salaam,Rukwa na Mtwara.



Kwa mujibu wa  Sr.Mgaya shule ya St.Vinsenti ilianzishwa mwaka 1984 na kanisa katoliki jimbo kuu la Songea baada ya kufanyika makubaliano kati ya kanisa na serikali.



“Makubaliano hayo yalifanyika baada ya kufanyika utafiti na kugundulika kuwa wapo watoto wengi viziwi katika ukanda ya kusini ambao wanakosa nafasi ya shule baada ya ukanda mzima wa kusini kutokuwepo kwa shule ya walemavu viziwi”,alisema.



Shule hiyo ilipata usajili Januari 15,1989 na kupewa namba RV/01/02/033 na ilifunguliwa  rasmi na waziri mkuu mstaafu hayati  Rashid Mfaume Kawawa Februari 2,1992 ambaye siku ya ufunguzi alipanda mti wa kumbukumbu ambao bado upo hadi leo.



Kulingana na Sr.Mgaya shule hiyo  ina uwezo wa kupokea wanafunzi wasiozidi 200 tu na kwamba kutokana na hali hiyo Kila mwaka watoto wanye ulemavu viziwi wengi wanakosa nafasi ya kujiunga katika shule hiyo kutokana na shule kukosa uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi ya hao.



“kutokana na changamoto zilizopo idadi ya wanafunzi waliopo hivi sasa katika shule yetu ni 140 ambao wanasoma kuanzia  shule ya awali hadi darasa la saba”alisema na kuongeza kuwa shule hiyo ina kitengo cha ufundi katika fani za useremala,ushonaji,,upimaji na utengenezaji wa shime sikio kwa ajili ya viziwi.



Ameyataja  baadhi ya mafanikio yaliopatikana tangu kuanzishwa kwa shule hiyo kuwa ni shule kujitosheleza katika majengo na samani,vifaa vya kujifunzia na kufundishia mazingira mazuri ya kujifunzia,kufundishia na nyumba za walimu zinazokidhi mahitaji ya walimu.



Sr.Mgaya amesema shule hiyo inafanya vizuri kitaaluma ambapo kila mwaka karibu wanafunzi wote wanachaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule zinazochukua wanafunzi wenye ulemavu zikiwemo za Njombe na Iringa.



 “Kwa mfano matokeo ya mwaka juzi ya darasa la saba yanaonesha kuwa wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 19,wanafunzi wote walifaulu, shule yetu ngazi ya wilaya ilishika nafasi ya saba kati ya shule 75,kimkoa ilikamata nafasi ya 78 kati ya shule 729 na kitaifa shule ilikuwa ya 1854 kati ya shule 15,867’’,alisema.



Shule hiyo ina kitengo  cha ufundi ambacho  kinatoa mafunzo ya awali katika fani za useremala na ushonaji na kufanya mitihani ya VETA na kupewa  vyeti vya ufundi kila mwaka.



Pia Shule hiyo imeanzisha darasa la kompyuta ili kuendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia kutokana na ukweli kuwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wana uwezo mkubwa katika masomo ya vitendo hivyo wanaweza kufanya vizuri  katika somo hilo.



Hata hivyo shule kwa ajili ya watu wenye ulemavu hapa nchini bado ni changamoto kubwa kutokana na ukweli kuwa hadi sasa kuna shule chache tena nyingi zinamilikiwa na taasisi binafsi na mashirika ya dini licha ya kwamba idadi ya watu wenye ulemavu inaendelea kuongezeka.



Kwa mfano Halmashauri ya manispaa ya Songea ina shule 10  zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum kati ya hizo shule moja  ni ya sekondari ambayo ni shule ya wavulana Songea na vitengo nane  katika shule za  msing za serikali na shule moja ya mtakatifu Vincenti inayomilikiwa na kanisa katoliki.



Kaimu afisa elimu wa manispaa ya Songea Sunday Wahyungi amezitaja shule za msingi zenye vitengo vya elimu maalum kuwa ni Luhira, Chandarua, Mitawa, Mahiro, Ndilimalitembo, Subira,Mfaranyaki na Chemchem.



kulingana na takwimu za idara ya elimu ya manispaa hiyo hadi kufikia mwezi Mei,2016 katika shule hizo kuna jumla ya wanafunzi 328 wenye ulemavu wa aina mbalimbali ukiwemo viziwi, ngozi, akili,viungo na wanafunzi wenye ulemavu zaidi ya mmoja.



Takwimu za wenye ulemavu katika mkoa wa Ruvuma kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa  kuna watu 523 wenye ualbino,wasioona zaidi ya 20,000,viziwi zaidi ya 12,000,wenye ulemavu wa viungo zaidi ya 15,000,,wenye ulemavu wa akiri 14,000 na wenye aina nyingine za ulemavu karibu 5000.



Tanzania imekuwa na ongezeko kubwa la  watu wenye ulemavu  wa aina mbalimbali ambao wanahitaji mahitaji maalum ya elimu,miundombinu pamoja na mahitaji mengine.



Kulingana na sensa hiyo Tanzania ina zaidi ya watu 16,000 wenye ualbino,wasioona zaidi ya 848,000,viziwi zaidi ya 425,000,ulemavu wa viungo zaidi ya 525,000,ulemavu wa akiri zaidi ya 400,000, na karibu 100,000 wana ulemavu wa aina nyingine.



Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo ambaye amebobea katika masuala ya elimu,mazingira,madini,gesi na mafuta anapatikana kwa simu 0784765917,baruapepe albano.midelo@songeamc.go.tz

          


No comments:

Post a Comment