MIAKA mitano ijayo
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
inatarajiwa kuwa kituo kikubwa cha utalii katika ukanda wa kusini.
![]() |
| Leonidas Gama mbunge wa Songea mjini |
Ofisa habari wa
manispaa hiyo Albano Midelo alisema mbunge wa Songea mjini Leonidas Gama
akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa manispaa ya Songea kwenye ukumbi wa
manispaa hiyo alisema hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu barabara ya kutoka
Mtwara hadi Mbinga inatarajiwa kuwa lami.
Gama amesema mara
baada ya barabara hiyo kukamilika fursa za uwekezaji hasa katika sekta ya
utalii zilizopo manispaa ya Songea zitavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje
ya nchi na kufika kuwekeza hali ambayo itaongeza mapato na ajira kwa wakazi wa
manispaa hiyo.
“Mtwara kuna wawekezaji ambao wapo kutokana na kugundulika gesi,wawekezaji hawapendi joto
hivyo watapenda kutembelea maeneo yenye hali nzuri ya hewa kama Songea ili
kutalii,hivyo fursa za utalii zilizopo manispaa ya Songea zitaongeza
uwekezaji’’, alisema Gama.
Gama amesema
mazingira ya Songea kutokana na hali ya hewa na vivutio adimu vya utalii
itakuwa ni kituo kikuu cha utalii hivyo kufungua milango ya utalii kusini
kuanzia Mtwara hadi mwambao mwa ziwa
Nyasa.
Kutokana na hali hiyo
amewataka watalaam wa manispaa ya Songea kuanza kuboresha vivutio ambavyo
vitawavutia wawekezaji hasa ujenzi wa hoteli bora,nyumba za kulala
wageni,miundombinu bora ya umeme,kuboresha kiwanja wa ndege cha Songea pamoja
na kuvitangaza vivutio vyote vya utalii vilivyopo.
“Ingieni kwenye
mtandao,tafuteni fursa za uwekezaji zipo.Kwa mfano wajerumani ni wawekezaji wazuri ambao
wanaangalia fursa na kukutafutia wawekezaji moja kwa moja,hivyo Songea
tuwatumia hao ili kuendeleza sekta ya utalii ambayo inachangia pato la Taifa’’,alisisitiza.
Mchumi wa manispaa ya
Songea Raphael Kimary anavitaja vivutio adimu vya utalii vilivyopo katika
manispaa hiyo kuwa ni makumbusho ya
Taifa ya Majimaji,hifadhi ya asili ya
Luhira na vivutio vingine vya kishujaa na kiutamaduni.
“Manispaa
ya Songea ni chanzo cha bonde la Mto
Ruvuma ambao unatiririsha maji katika baharí ya Hindi na Mto Ruhila ambao
hutiririsha maji katika ziwa Nyasa.Mtiririko wa maji ya mito hutegemea majira
ya mwaka, huwa mengi wakati wa mvua’’,alisema Kimary.
Hata hivyo amesema Sehemu kubwa ya Manispaa ya
Songea ina umbile la tambarare, mwinuko
wa Milima Matogoro na Unangwa na kwamba Manispaa ipo katika mwinuko wa nchi
kutoka usawa wa baharí kati ya mita 980 na 1500.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni miongoni mwa
Halmashauri tatu zilizopo katika wilaya ya Songea ikiwa na kata 21 na mitaa 95.Halmashauri
nyingine zinazounda wilaya hiyo ni Halmashauri ya wilaya ya Songea na Madaba.
Mwisho

No comments:
Post a Comment