Thursday, July 21, 2016

Watu 21,000 Songea wanaishi na VVU

Watu 10,000 wanatumia ARVS

MRATIBU wa UKIMWI na tiba katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Felista Kibena amesema zaidi ya watu 21,000 katika manispaa ya hiyo wanaishi na virusi vya UKIMWI.
Felista Kibena

Ofisa habari wa manispaa hiyo Albano Midelo amesema,Kibena alitoa takwimu hizo wakati anatoa  mada ya ukweli kuhusu virusi vya UKIMWI  na ugonjwa wa UKIMWI kwa watumishi wa manispaa hiyo mafunzo ambayo yamefanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa manispaa ya Songea.

Kwa mujibu wa Kibena kati ya watu wenye virusi,watu zaidi ya 10,000 ndiyo wanaugua ugonjwa wa UKIMWI na kutumia dawa za kurefusha maisha za ARV na kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika manispaa ya Songea ni asilimia nne.

Hata hivyo amesema mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa ukiwa na maambukizi ya asilimia saba ambapo mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza kitaifa ukiwa na asilimia  14.5,nafasi ya pili inashika na mkoa
wa Iringa,ikifuatiwa na mkoa wa Mbeya kwa nafasi ya tatu na mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya tano.

“Kiwango cha maambukizi katika mkoa wa Ruvuma kinapanda kwa kasi awali kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia tano lakini sasa ni asilimia saba,tumevuka kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia tano’’,alisema.

Hata hivyo amesema maambukizo makubwa ya virusi vya UKIMWI hivi sasa yanachangiwa na makundi maalum ambayo aliyataja kuwa ni watu wanaofanya ngono kinyume cha maumbile,watu wanaofanya biashara ya ngono,wafungwa na watumiaji wa madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano au kubwia.

Kibena alisema maambukizo ya virusi katika makundi maalum yamefikia asilimia 36 ambapo kila watu 100 watu 36 wana virusi vya UKIMWI ukilinganisha na kiwango cha kitaifa cha asilimia tano ambayo ni sawa na kila watu 100 watano wana virusi.

Amezitaja kata ambazo zinaongoza kwa maambukizo ya virusi vya UKIMWI katika manispaa ya Songea kuwa ni Bombambili, Mateka,Ruvuma na Lilambo.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2013 hapa nchini watu milioni moja na nusu walikuwa wanaishi na virusi ambapo kwa mwaka 2014 pekee takwimu zinaonesha kuwa katika Tanzania watu 74,000 wameambukizwa virusi na zaidi ya watu laki tano walikuwa wanatumia dawa za ARV ambapo hadi sasa watu zaidi ya laki sita wanatumia ARV.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Afya Duniani  watu milioni 35 wanaishi na virusi vya UKIMWI hadi kufikia mwaka 2013 kati yao  watu milioni 24 sawa na asilimia 71 walitoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambapo watu milioni moja na nusu wamekufa hadi kufikia mwaka 2013 na watu milioni 12 wanatumia dawa za ARV.

MWISHO

No comments:

Post a Comment